Ujumbe kutoka kwa Afisa Mkuu Mtendaji

Sisi ni shirika endelevu na la uvumbuzi lililolainishwa na lengo letu kuu la Kubadilisha Maisha. Ni lengo hili, pamoja na matumizi yetu ya teknolojia, ambalo hutuwezesha kuunda bidhaa zinazojibu mahitaji ya wateja wetu na kutoa suluhisho kwa changamoto zinazokabili jamii. Hatua yetu ya kukumbatia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, ambapo tumefungamanisha malengo tisa kwenye fikira na matendo yetu, imetusaidia kuwa wa manufaa kwa jamii tunazohudumia.

Huwa tunajizatiti kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma – iwe ni kupitia kuundwa kwa jamii ya dijitali iliyo na mtazamo wa kisasa, kwa kutoa majukwaa ya ufadhili wa ununuzi wa vifaa na mitambo kwa mfano Lipa Mdogo Mdogo. Huwa tunawawezesha wateja wetu kupanua wigo wao na fursa zao kupitia intaneti, au kwa kufanya kazi kuhifadhi maliasili kupitia mikakati kama vile upanzi wa miti milioni moja kama sehemu ya lengo letu la kuhakikisha tunakuwa kampuni isiyochangia ongezeko la gesi ya kaboni kwenye mazingira kufikia mwaka 2050.

Kwa kweli, tunaimarisha uhusiano huu na jamii zetu kupitia uwekezaji wa kijamii tunaoufanya kupitia Nyakfu zetu mbili na pia udhamini unaofanywa na nembo yetu. Juhudi hizi, pamoja na utekelezaji mwema wa mkakati wetu, vimetuwezesha kuandikisha matokeo mazuri ambayo tunayo sasa.

Nguvu za mkakati wetu

Mwaka wa kwanza wa mkakati wetu mpya, ulioidhinishwa na Bodi mwaka wa kifedha wa 2020, umeonesha matokeo ya kufurahisha, kwa kutuwezesha kuwa shirika la kidijitali linalowathamini wateja, na kutuwekea msingi imara wa Kundi siku za usoni na pia tumepiga hatua kubwa katika kila vitengo vya biashara yetu.

Tumeshuhudia ukuaji sawa katika vipimo vyetu vya ufanisi katika utoaji huduma kwa wateja, na pia vipimo vinavyohusu shughuli zetu za kibiashara. Kwa kuendelea kuwapa kipaumbele wateja, azma yetu katika mwaka huu mpya wa kifedha ni kuongeza kasi maeneo mapya ya ukuaji, na kutoa huduma ya hali ya juu kwa wateja, kwa kuendana na lengo letu la kuwa kampuni ya teknolojia inayoongozwa na malengo kufikia mwisho wa mwaka 2025.

Katika kuufuata mkakati huu, tutaendelea kutafuta washirika wapya pamoja na watu tunaoweza kushikana, kuunganisha kampuni zao na zetu au kuzinunua (M&A), tunapopanua shughuli zetu na kuingia kwenye maeneo ambayo hatujayazoea sana – lakini kama kawaida, bila shaka, kupitia mashauriano mema na ya thamani na mamlaka.

Kudhibiti hatari

Mtazamo wetu katika kudhibiti hatari umefungamana na mkakati wetu – hasa hatari inayotokana na mamlaka na sheria tunapokuza biashara yetu ya mawasiliano, na pia hatari ya utekelezaji tunapopanua shughuli zetu hadi Ethiopia. Kadhalika, tumeendelea kufuatilia kwa makini mazingira mapana ya kiuchumi yanayodorora – licha ya kujikwamua kutoka kwa COVID-19 na huku 2022 ukiwa mwaka wa uchaguzi Kenya, pamoja na kuzuka kwa vita vya Urusi na Ukraine. Tishio la usalama wa data na usalama wa mtandaoni ni mambo mawili pia ambayo yanaendelea kuibua wasiwasi, na tumejitolea kuendelea kuyafuatilia kwa karibu.

Bado tuna imani katika mfumo wetu wa kusimamia hatari na tunaelewa umuhimu wa kuongoza ukakamavu wa kibiashara kutoka kwa mtazamo wa usimamizi na udhibiti wa hatari.

Kutimiza ruwaza yetu

Katika mwaka tunaouangazia, tulifanikiwa kuhamia katika mfumo wa kufanya kazi kwa wepesi, wenye nguzo yake katika utamaduni unaoongozwa na teknolojia ambapo tunasaidiwa na utaalamu wa teknolojia tulioustawisha. Hatua kubwa tulizozipiga katika hili ni kutumiwa kwa mashine, mitambo na digitali katika maeneo mengi ya biashara yetu, kuiboresha M-PESA na kuifanya mfumo wa pande mbili wa kidijitali unaohudumia biashara na pia wateja wa kawaida. Tumewekeza pia katika data na utathmini wake ili kuunda bidhaa mwafaka zaidi.

M-PESA ilisherehekea miaka 15 ya utoaji huduma ya kipekee kama kiungo imara cha huduma za kifedha na teknolojia katika biashara yetu. Pamoja na kutekeleza programu tumishi zake mbili kwa mafanikio, M-PESA iliandikisha ongezeko la 63.4% la wafanyabiashara wanaoitumia katika mwaka huo, na kufikisha idadi ya jumla kuwa karibu 500,000. Biashara zaidi ya 150,000 sasa zinajivunia kuonekana zaidi kwa shughuli zake, na wanaendesha shughuli zao moja kwa moja kupitia huduma ya till, na huduma hii ya malipo inapatikana kote nchini.

Mafanikio mengine makuu mwaka huo, ambapo tulipunguza pengo la kidijitali miongoni mwa wateja, ni pamoja na vituo 567 vipya vya kusambaza mawimbi ya 4G kote nchini, 800 km za nyaya za faiba, na juhudi zetu za kufanya simu na vifaa vinavyotumia 4G kupatikana kwa bei nafuu kwa watu wengi zaidi iwezekanavyo.

Kadhalika, tumewasaidia wateja kuongeza matumizi yao ya data kwa zaidi ya 275%, ambapo kwa kadri mapato kutoka kwa kila mteja (ARPU) yameongezeka kwa zaidi ya 175%, na huduma yetu ya Lipa Mdogo Mdogo imesaidia sana katika hili. Aidha, huduma yetu ya Pochi la Biashara imeongeza mtandao wa biashara zinazotumia huduma zetu hadi 3.2 milioni.

Bidhaa mpya kwa maeneo mapya ya ukuaji

Kwa pamoja, mkakati wetu na kuweka mteja mbele katika kila jambo, vimetusaidia kuanzisha huduma na bidhaa bora zaidi, kwa mfano Nyoosha Shillingi, mpango wa malipo ya data unaotoa thamani zaidi kwa mteja kwa bei ile ile; na Halal Pesa, iliyozinduliwa kwa ushirikiano na benki ya Gulf African Bank, inayotoa huduma ya kifedha kidijitali ikifuata Sharia. Katika mkakati mwingine wa uvumbuzi, tumeanzisha kadi ya Visa ya mtandaoni ya M-PESA GlobalPay, ya kuwezesha malipo ya nje ya nchi kupitia mtandao. Tunapanga pia, iwapo tutapata idhini kutoka kwa mamlaka, kuzindua huduma ya M-PESA junior ili kupanua utoaji wa huduma za kifedha kwa Watoto walio na simu za kisasa.

Matokeo ya kujivunia:

Matokeo ambayo tumeandikisha mwaka huu yanajieleza yenyewe:

Bila kujumuisha Ethiopia:

  • Mapato kabla ya Riba na Ushuru (EBIT), ni KShs 114.3 bilioni, ukilinganisha na makadirio ya KShs 107–110 bilioni
  • Matumizi kwenye Mtaji (Capex) yalifikia KShs 39.3 bilioni dhidi ya makadirio ya KShs 40–43 bilioni

Ukijumuisha Ethiopia:

  • EBIT ni KShs 109.1 bilioni, dhidi ya makadirio ya KShs 97–100 bilioni
  • Capex yalifikia KShs 49.8 bilioni, dhidi ya makadirio ya KShs 70–73 bilioni

Kwa maelezo zaidi kuhusu fedha na matokeo yetu dhidi ya mkakati, tazama kurasa 106 na 114 mtawalia.

Wadau wetu

Tunatambua umuhimu wa kutilia maanani maoni ya wadau wetu kuhusu huduma zetu na kushauriana nao kikamilifu. Ni kiungo muhimu katika ustawishaji wa mkakati wetu, kama ilivyo pia kwa bidhaa na huduma tunazotoa. Kile wateja wetu wanachohitaji, mahitaji ya mamlaka zinazosimamia sekta yetu, na mahitaji ya jamii zetu, ni mambo ambayo huwa mbele akilini mwetu tunapobadilika na kuwa shirika linalothamini na kuangazia sana mteja, na linaloweka dijitali mbele.

Kuhusiana na hili, tumefanya utafiti wa kina sokoni, kufanyisha utafiti wa kila mwezi wa vipimo vya uwezekano wa wateja kutupendekeza kwa wengine (NPS) na kudumisha mawasiliano ya mara kwa mara na yenye tija pamoja na mashauriano na mamlaka na washirika kuhakikisha tunatimiza masharti yote ya kisheria na kujibu masuala yanayoibuka.

Kwa wafanyakazi wetu, tulifanya utafiti wa kina hasa wakati wa janga la corona. Hii ilikuwa kuhakikisha kwamba wanawezeshwa kutoa huduma ya ubora wa kiwango kinachohitajika, na kufanya kazi kutoka manyumbani mwao, tukizingatia pia afya yao ya kimwili na kiakili. Tunatafuta pia ushirikiano wa kukuza wataalamu wa kiteknolojia tunapobadilika na kuwa shirika la dijitali kwanza na ambalo mahitaji yake ya utaalamu na ujuzi yanaongezeka.

Kupitia Nyakfu zetu mbili, huwa tunadadisi kwa makini uwekezaji wetu wa kijamii, ili kuhakikisha mahitaji na jamii katika maeneo tunayofanya kazi yanatimizwa.

Kadhalika, kama mlipaji ushuru mkubwa zaidi nchini, tunafahamu vyema vipaumbele vya serikali. Katika mwaka tunaouangazia, tulidumisha uhusiano mzuri na wa maana na serikali kama mdau muhimu. Tumejitolea kwa utawala wa uwazi na uwajibikaji ndani ya shirika letu, pamoja na kufuata kikamilifu kanuni na sheria zote, kwa maslahi mema ya taifa katika mazungumzo na mashauriano yetu.

Kutoka kwa mtazamo wa utoaji wa bidhaa na huduma, tumezingatia thamani ya pamoja, tukiwa tumejitolea kuendeleza kukumbatiwa kwa watu wa asili mbalimbali na kujumuishwa kwa watoaji bidhaa na huduma za ndani na nje ya nchi kuhakikisha kwamba sio wao pekee, bali pia jamii pana maeneo wanayohudumu, zinafaidi.

Mawasiliano yetu na Bodi na wenyehisa yameendelea kuwa ya mara kwa mara, ambapo ripoti zimetolewa kwa wakati, na mawasiliano yamekuwa ya uwazi na uwajibikaji pia. Mawasiliano na uhusiano wetu na Bodi na kamati zake, vimetoa mfumo mzuri unaohakikisha kiwango cha juu zaidi sio tu cha utawala bali pia ushauri.

Upanuzi kwenye kanda

Kukabidhiwa leseni ya mawasiliano Julai 2021 kuanza shughuli zetu Ethiopia kumetufungulia milango mipya. Kila kitu kiko tayari kwa uzinduzi 2022. Tumefanikiwa kufanya mashauriano na kujadili changamoto zisizotarajiwa zilizokuwa zimeibuka tangu kukabidhiwa leseni. Kiwango cha juu cha mfumko wa bei na kuyumba kwa ubadilishanaji wa fedha za kigeni bado vimesalia kuwa mambo tunayofuatilia kwa karibu na kuyatafutia suluhu. Licha ya hayo, tumepiga hatua kubwa kwa usaidizi kutoka kwa Serikali ya Ethiopia na Mamlaka ya Mawasiliano ya Ethiopia (ECA).

Usaidizi huu umewezesha kusajiliwa kwa kampuni, kupatikana kwa idhini ya kuweka minara ya kusambaza mawimbi ya simu, kujenga vituo viwili vya data, na hatua ya kihistoria ya kupiga simu ya kwanza ya majaribio kupitia mtandao wetu, kutuma SMS yetu ya kwanza, na kutumia data pia mara ya kwanza.

Baada ya kuajiri kundi la wafanyakazi zaidi ya 300 wenye ujuzi, ambapo 55% ni wenyeji, lengo letu ni kuongeza wafanyakazi wetu huko hadi 1,000 katika mwaka wa kifedha wa 2023. Tumewachukua wasambazaji 29, tukapata maeneo manne ya kufungua maduka ya reja reja, na tumetoa zabuni kwa kituo kimoja cha mawasiliano na huduma kwa wateja jijini Addis Ababa.

Tumepiga hatua pia na Ethiotel katika kujenga ushirikiano wa faida kwa pande zote mbili wa kuunganisha mawasiliano na pia uwezo wa kusambaza mawimbi ya mawasiliano, pamoja na kugawana minara ya mawasiliano na umeme. Kadhalika, tunaendelea kushauriana na Serikali ya Ethiopia kuhusu mambo yanayohitajika ili kutuwezesha kuanza biashara ya huduma ya kutuma na kupokea pesa kwa njia ya simu nchini humo.

Tukisonga mbele

Katika kipindi kifupi, kipaumbele chetu katika mwaka wa kifedha 2023 kitakuwa kuunda biashara thabiti katika maeneo mapya ya ukuaji Kenya na nje ya nchi, kwa lengo la kutumia kwa pamoja nguvu ya teknolojia mpya na uvumbuzi kukuza zaidi biashara yetu ya mawasiliano na malipo. Katika hili, lengo letu ni:

  • Kuungana na kampuni nyingine na ununuzi wa kampuni nyingine (M&A), pamoja na leseni na ubia kuwezesha ukuaji na kuongoza uwekezaji wetu
  • Kupanua huduma za mtandao wa nyaya manyumbani za Fibre to the Home (FTTH) na Fibre to the Building (FTTB)
  • Kutumia vyema zaidi teknolojia ya faiba na 5G, mwanzo ikiwa mtandao usiotumia nyaya manyumbani
  • Kupanua huduma zetu za kifedha, kwa kutegemea kukamilishwa kwa ushirikiano unaohitajika na idhini ya mamlaka, kuingia katika huduma kama vile bima, mali na biashara ya mtandaoni kwa wateja na SMEs
  • Kupanua huduma kadha za dijitali, hasa AgriTech na Digital Health, pamoja na kuweka muundo bora zaidi wa kufanya kazi na ushirikiano ili kupanua teknolojia ya kutumia mtandao kuunganisha mitambo na vifaa yaani Internet of Things (IoT) na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT)
  • Kukuza huduma za kidijitali kama vile maudhui, elimu, na matangazo ili kuongeza utamaduni wa watu kutumia data zaidi

Shukrani

Ningependa kwanza kuwashukuru wateja wetu kwa kutuunga mkono na imani yao katika biashara yetu. Tunaahidi kuendelea kuangazia zaidi mahitaji yenu na kuwawezesha kutimiza matamanio na ndoto zenu kupitia bidhaa na huduma zetu. Ni lazima bila shaka niishukuru Bodi – ushauri wao wa busara na hekima, uungaji mkono wao wa mkakati wetu, na uongozi wao wa shirika, ni vya thamani kubwa, na kiungo muhimu kwa ufanisi wetu.

Shukrani zangu pia ni kwa wafanyakazi wetu wapatao 6,000, pamoja na washirika, wasambazaji wa bidhaa na huduma zetu, na mawakala tunaofanyakazi nao. Mfumoikolojia unaowajumuisha wao pia hufaidi watu zaidi ya milioni moja kwa njia moja ama nyingine na ni muhimu sana katika kutimizwa kwa malengo ya mkakati wetu.

Ningependa pia kuzishukuru Serikali za Kenya na Ethiopia kwa uungaji mkono wao katika kuhakikisha kwamba tupo katika nafasi nzuri ya kutoa msingi wa kuunda na kustawisha biashara ya kidijitali inayowawezesha watu binafsi, biashara na mataifa husika katika mawasiliano, fedha kwa njia ya simu na mengine mengi zaidi.

Tunasubiri kwa hamu kuendelea kufanya kazi na watu hawa wote muhimu, asasi na mashirika pia tunaposonga mbele kwa pamoja kwenye siku zijazo.

Peter Ndegwa
Afisa Mkuu Mtendaji