Ujumbe kutoka kwa Mwenyekiti

Kwa ufupi

Bodi imefurahishwa na ukakamavu ambao biashara yetu imedhihirisha katika mwaka uliomalizika na mwelekeo wa kuimarika tena kwa uchumi ambapo kiwango cha ukuaji wa pato la taifa yaani GDP kimezidi kiwango cha kabla ya janga la corona.

Katika uchumi ambao unazidi kuwa wa kidijitali, tumejitolea kuisaidia Serikali ya Kenya na raia wa Kenya katika kupitia kipindi hiki cha kujikwamua. Ili kudumisha ukakamavu wa biashara yetu, ni lazima tuendelee kuvumbua na kutekeleza kwa kasi huduma endelevu za kukidhi mahitaji ya kidijitali ya wateja wetu.

Kundi letu sasa lipo katika mwaka wa pili wa utekelezaji wa mkakati wa miaka mitano unaoongozwa na lengo la kubadilisha Maisha. Bodi inaendelea kuunga mkono wasimamizi katika mipango yao ya biashara, ambapo kulipatikana mafanikio makubwa mwaka huu wa kifedha. Tumefurahishwa na matokeo mazuri ya kifedha ya biashara yetu, ambayo imeshuhudia ukuaji thabiti wa mapato, kuongezeka kwa thamani kwa wenyehisa na tunaendeleza nafasi za kazi zaidi ya milioni moja kote nchini. Matokeo yake yamekuwa ni kuinuliwa kwa jamii, na, kwetu kama shirika, uwajibikaji zaidi kwa wenyehisa wetu, wawekezaji wetu, na kwa jamii yetu.

Mkakati wa kuinuka

Tumemaliza miaka miwili sasa ya utekelezaji wa mkakati wetu wa miaka mitano, na mafanikio yake ni dhihirisho tosha ya azma yetu kuu ya kuwaweka wateja mbele katika jambo lolote tulitendalo. Msingi huu ni kiungo muhimu katika kujitolea kwetu, kama inavyodhihirishwa na shughuli za Nyakfu zetu mbili, katika kuendelea kutoa mchango wa maana kuhakikisha ulimwengu endelevu na siku za usoni endelevu.

Tunajivunia kwamba katika kutimiza lengo hili, wakfu wa M-PESA Foundation, miongoni mwa miradi yake mingine, kwa ushirikiano na Kaunti ya Kwale na Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya, wameweka pampu ya maji inayotumia kawi ya jua katika Bwawa la Nyalani. Mradi huu utawezesha zaidi ya wakazi 22,000 wa kaunti hiyo kupata maji safi kwa ajili ya matumizi yao ya nyumbani. Kadhalika, pampu hiyo itawezesha unyunyiziaji maji katika ardhi ya ekari 105 katika kaunti hiyo, na hivyo kuimarisha uzalishaji wa chakula kwa njia ya moja kwa moja.

Vilevile, kama sehemu ya kujitolea kwetu kuunda thamani ya pamoja, Wakfu huo umeshirikiana na Hospitali ya Watoto ya Gertrude kuzindua Daktari Smart, ambayo ni huduma ya afya ya njia ya simu ambayo itatoa matibabu maalum kwa watoto zaidi ya 32,000 katika kaunti za mbali katika kipindi cha miaka mitatu.

Kadhalika, sasa tunashiriki katika kampeni ya Pamoja Tuungane, mkakati ambao, baada ya kuanzishwa katika mwaka wa kifedha wa 2022, unawahamasisha Wakenya kutoa msaada wa alama zao za Bonga au pesa taslimu kusaidia watoto na familia zilizoathiriwa na ukame. Tumeahidi kutoa vyakula vya thamani ya Kshs100 milioni vitakavyosambazwa katika kaunti 23 zilizoathirika zaidi.

Kufuatilia mazingira yetu ya uendeshaji shughuli

Mwaka tunaouangazia ulijaa mabadiliko makubwa na hali ya kipekee, hata ukizingatia kuimarika tena kwa uchumi ambako tumeanza kushuhudia. Bodi liliendelea kutathmini hatari za kibiashara zilizotokana na siasa za kanda, matukio ya kiuchumi na wasiwasi kwenye sekta yenyewe, pamoja na hatari zilizoathiri sifa zetu kama kampuni.

Tumeshuhudia, katika mwaka huo, changamoto mpya zilizotokana na maagizo mapya ya mamlaka, kufanyiwa mabadiliko kwa ada za upigaji simu kwenye mitandao mingine (MTRs), pamoja na ongezeko katika kodi ya GSM. Pia, utekelezaji wa mabadiliko katika njia za kuwapata wateja ikiwa ni pamoja usajili wa wateja. Tuliendelea kuwaunga mkono wasimamizi walipoendelea kujadiliana na mamlaka kuhakikisha tunafuata mahitaji ya usajili, ushuru na sheria zilizopo.

Huku kampeni za uchaguzi mkuu wa Agosti zikiendelea, tutaendelea kufuatilia kwa karibu hatari za kisiasa zilizo na uwezo wa kuathiri biashara yetu katika upande wa shughuli zetu na pia miundo mbinu yetu.

Licha ya changamoto hizi, kumekuwepo na ukuaji mzuri wa GDP wa 7.5% katika mwaka 2021 kiwango ambacho kimezidi kiwango cha kabla ya COVID-19. Tunatazama hii kama fursa ambayo inaweza kutumiwa vyema, hasa na biashara ndogo na za wastani yaani MSMEs.

Matokeo ya Bodi

Inafurahisha kuweza kueleza kuwa Bodi na kamati zake zote wamefanya vyema sana, sio tu katika kutekeleza majukumu yao, bali pia katika kuunga mkono na kusaidia wasimamizi, kupokezana majukumu kwa uwajibikaji na uwazi, na kwa kutumia ujuzi na utaalamu wao kwa pamoja kukabiliana na changamoto zilizokuwepo. Kadhalika, kutumia vyema fursa zilizojidhihirisha katika mwaka huo.

Pia, wakati wa mwaka huo tunaouangazia, tuliendelea kufanya kazi kwa bidii kuelewa vyema maswali na maoni yaliyotolewa na wadau wetu, na kuyapokea na kuyashughulikia ili kuhakikisha mkakati wetu sio tu kwamba unaendana na ruwaza, ndoto na lengo letu, lakini pia mahitaji ya watu binafsi na mashirika yote yanayoathiriwa na shughuli zetu.

Shukrani

Ningependa kuwashuruku wenzangu kwenye Bodi kwa jitihada zao na kujitolea kwao mwaka huo katika kutoa utathmini wa maana na ushauri muhimu wa kufuatwa na wasimamizi. Ujuzi wao, busara na uzoefu vimeongeza thamani sana kwenye Kundi na vilichangia si haba katika ufanizi wake FY2022.

Ninamshukuru sana pia Afisa Mkuu Mtendaji wetu Peter Ndegwa na kundi lake la wasimamizi kwa uongozi wao wa kipekee na kwa walivyoelekeza biashara yetu kuunda thamani kupitia matokeo mazuri na ya kuridhisha tuliyoyaandikisha.

Mwisho, kwa wadau wetu, na hasa serikali na mamlaka zinazosimamia sekta yetu ambazo huwa tunajadiliana na kushauriana mara kwa mara, tungependa kusema kuwa tunashukuru sana kwa usaidizi wao na kwa kujitolea kwao kushauriana nasi tunaposonga mbele na kujenga siku za usoni bora hata zaidi kwetu sote.

Michael Joseph
Mwenyekiti